FAHAMU HUDUMA YA UTOAJI MAPEPO (EXCORCISM) KATIKA
KANISA KATOLIKI.
Na
Wilehard
Maro
Niliye mdogo kuliko wote.
Lipo swali au shutuma juu
ya kanisa katoliki kuwa “wakatoliki hawatoi mapepo kama alivyofanya Yesu” basi
leo tuichambue huduma hii katika kanisa katoliki. Kwanza ni wazi kuwa kanisa
katoliki linatoa huduma hii kwa waamini wanaothibitika kushikiliwa na nguvu za
kishetani (demonic possession) kwa kuondoa nguvu hizo kwa jina la Yesu. Katekisimu
ya Kanisa Katoliki namba 1673 inaeleza kuwa kupunga pepo kunaelekezwa katika
kumfukuza shetani au ukombozi dhidi ya kupagawa na pepo na kupitia kwa mamlaka
ya kiroho ambayo Kristo amelikabidhi Kanisa. Mara nyingi huduma hii haifanyiki
kwa uwazi au mbele ya kusanyiko kama ilivyo kwa baadhi ya madhehebu ya kipentekoste
na kiprotestanti hivo kufanya ionekane kama huwa haifanyiki lakini ni kweli
kuwa huduma hii inafanyika ndani ya kanisa katoliki.
1. Kupunga
pepo kulianza lini?
Visa vya kupunga pepo ni
vya zamani kabla na baada ya Yesu, ila katika utaratibu wa kanisa, mwaka 1614,
kanisa lilitoa mingozo rasmi juu ya upungaji pepo. Karne ya 15, walei na
mapadre walipunga pepo, wote walihesabiwa kuwa wana nguvu na mamlaka hayo na njia
ya Kibenectine iliyojilikana kama "Vade
retro satana" ilitumiwa kwa lugha yetu “rudi
nyuma, shetani”. Mwaka 1999 miongozo hiyo ya upungaji pepo ilipitiwa upya
kutokana na kuongezeka kwa mahitaji. Utaratibu huo ulitolewa kuweka maelekezo
ya namna ya mtu anayedai kuwa na mapepo atafwata ili kupata huduma hii,
ikijumuisha uchunguzi wa kitabu unaofanywa na wataalamu wa magonjwa ya akili.
2. Nani
anatoa mapepo?
Ni muhimu kutambua kuwa
huduma hii ni ya masakramenti ila si sakramenti (sacramental but not a sacram).
Hivyo kanisa limeelekeza wazi kwa sheria zake (canon law) namba 1172 namba
mbili kinaleza Padre mwenye uelewa na elimu ya nguvu hizo anaruruhisiwa kufanya
huduma ya kupunga pepo kwa ruhusa ya askofu wa Jimbo lake. Pia sharia hii
inkatza katika kifungu namba moja kuwa hakuna mtu mwengine anaruhusiwa ispokuwa
Padre. Hivyo ni wazi kuwa huduma hii inatolewa na wenye daraja tu, waumini wa
kawaida hawaruhusiwi. Mkuu wa Idara
Idara ya Ibada Takatifu na Masakramenti Kardinali Jorge Arturo Medina Estevez
anasisitza ya kuwa "Kuendesha ibada hiyo ya kupunga mashetani,"
anakazia, "lazima kuthibitishwe na kukubaliwa na Askofu wa Jimbo, ambako
kunaweza kutolewa kwa tukio maalum, au kwa njia ya kudumu kwa Padre aliye na
huduma ya kupunga mashetani Jimboni."
3. Nani
anapungwa mapepo.
Utaratibu wa kupunga
mapepo umewekwa na kanisa ili kutobebesha mzigo wagonjwa au watu wenye matatizo
ya kiakili kwenye huduma hii badala yake, wapate tiba za kitabibu. Kutokana na
uchache wa kesi za kweli, miongozo ya Vaticani ya mwaka 1999 inaeleza wazi kuwa
lazima madaktari wathibitishe kuwa mtu huyo hana matatizo yoyote ya afya ya
akili. Matatizo ya kimaisha, uchumi, mahusiano, afya, jamii, siasa na mengineyo
yanayowazonga wengi yanapelekea msongo wa mawazo na kufanya watu wengi
kutawaliwa na hisia mbaya na matatizo ya kiakili. Waafrica wengi wanatawaliwa
na woga dhidi ya uchawi na mara kadhaa wanapojikuta katikati ya msongo wa
mawazo na mara moja hofu ya uchawi inaingia na kujitengenezea akili kuwa
wanatekwa na nguvu za kipepo. Lakini kanisa linataka kuthibishwa kwa nguvu za
kipepo kabla ya huduma hii. Hivyo, anayethibitika tu ndiye atakayepewa huduma.
4. Je
zipo dalili za kuweza kuashiria mtu mwenye kuweza kuwa na mapepo?
Mtandao wa Wikipedia
unataja baadhi ya dalili ambazo si za kawaida na kama mtu anazo baadhi au zote
basi vyema kuangalia utaratibu jimboni kwako kupata huduma hii. Kuna kukosa au
kutokuwa na hamu ya kula, kujikatakata au kujichubua au kujing’ata Ngozi,
kuhisi chumba ni cha baridi, mabadiliko yasiyo ya kawaida ya mwili na uso na
mikao isiyo ya kawaida, kupoteza uwezo wa kujimiliki na kushambulia wengine,
kutoa sauti za ajabu, nguvu za ajabu au zisizo za kawaida, kuongea na kuelewa
lugha ambayo muhusika hajawahi kuijua kabla, ufahamu wa vitu ambavyo vimefichwa
au kutoonekana, kutabiri mambo ya badae, Chuki kubwa dhidi ya vitu vyote vya
kidini, kupata shida kuingia kanisani au kusikia neno Yesu, kufukuza vitu au
Wanyama. Zingatia kuwa kuwa na dalili moja si kigezo kamili na hata ziwepo basi
ni padre mwenye ruhusa ndiye atakayechukua jukumu la kuthibitisha au kukataa.
5. Mchakato
wa utoaji mapepo.
Kwanza muhusika atafungwa
au kuweka mahala ambapo hataweza kuwadhuru wengine au yeye mwenyewe kisha,
padre atafanya sala kumtoa mtu huyo mapepo. Muongozo wa kotoa mapepo unapatikana
katika hati ya vatikani ya De
Exorcismis et Supplicationibus Quibusdam na pia katika ibada cha madhehebu ya Kirumi. Mchatako huu
huenda usifanikiwe mara moja, bali kwa siku, wiki n ahata mwezi kwa muendelezo
wa sala ya kupunga pepo.
Kila jimbo lina uwezekano
wa kuwapo kwa padre mpunga mapepo hivyo waamini wanaodhani kuwa wanahitaji basi
wakaribie kuitafuta na ni vyema sana kukubali pale unapothibitika una matatizo
ya kiakili si mapepo. Tabia ya baadhi ya waamini kupunga mapepo si nzuri ni
kinyume na taratibu na ni wazi kesi nyingi za waamuni kutoa mapepo zinajikita
katika woga wa kurithi na matatizo ya msongo wa mawazo. Wanaoweza kuingiwa pepo
ni wale wasioungama kabisa, hawashiriki wala kutaka kushiriki sakramenti za
kanisa, pepo hawawezi muingia mtu msafi bali wanafuata mahali wanapoweza
kuishi. Silaha kubwa dhidi ya mapepo ni kuishiriki vyema sakramenti ya kitubio,
kusali mara kwa mara, kutumia vitu vyenye baraka, kupokea ekarist takatifu mara
kwa mar ana kuishi usafi wa moyo. Mapepo kumuingia mkristo si jambo jepesi kama
tunavyoweza kusikia au kuona kwa watu wengine. Katika mada hii, jiulize tu, kwa
nini wanaotolewa mapepo huko kwengine ni watu wa kipato cha chini, historia za
kukandamizwa na wanatokea kwenye jamii zenye kuamini ushirikina, kamwe mama
matajiri, watu wenye amani nautulivu huwakuti kwenye vurumai hizi? Lipo swala
ambalo kanisa liliona na kuweka utaratibu, wengine wanahitaji tu kupatanishwa
na ndugu zao wala si kuombewa kwani wanaishi na chuki moyoni, wengine wana
msongo wa mawazo na hawana ahueni. Yote haya ni matatizo tunayobakizia huduma
hii wakati huduma za ushauri toka kwa wataalamu ungetatua matatizo hayo.
Basi nawatakieni kila
jema katika kujilinda na upotofu wa sasa, na vyema sana waamini walei kuongeza
bidi ya kujifunza na kuchimba mafundisho badala ya kuketi tu tukilalama kanisa
limekosa hiki ama kile. Tuwaone mapadre pia kwa maelekezo mazuri. Asanteni.
sandedeo_o Alice Bryan Download
ReplyDeleteinfatisi